Home Lifestyle Tuyisenge Atua Gor, Atatosha Dalugani za Olunga?

Tuyisenge Atua Gor, Atatosha Dalugani za Olunga?

Katika uzinduzi wa wachezaji wapya 11 wa Gor Mahia Jumanne Februari 2, mshambulizi Jacques Tuyisenge alivutia jicho la kila shabiki wa klabu hiyo aliyefika katika uga wa kitaifa wa Nyayo, Nairobi. Kwa wanahabari waliofika jicho la tathmini na kumweka mizanini lilikuwa dhahiri, uwezo wake ukilinganishwa na washambulizi watangulizi wake Michael Olunga na Meddie Kagere waliosanzuka.

Milioni nne pesa za kumhamisha raia huyo wa Rwanda kutoka Rwanda Police, ni mojawapo wa vigezo vinavyoweza kutumika kuashiria uwezo wake, lakini bado sana mpaka ajitose uwanjani kutetea dau hilo kubwa la usajili. Mbona milioni nne? Tuyisenge ni nahodha wa timu ya taifa ya Rwanda Amavubi Bees, na kufikia wakati wa kuhama klabu yake ya awali amekuwa nahodha pia. Kutajwa nahodha wa timu ya taifa ni ishara ya ukomavu na kutulia kimchezo, jambo analotarajiwa kuleta Ko’gallo.

 

Jacques Tuyisenge, kabla ya kujiunga na Gor. Amezinduliwa rasmi na Gor Mahia Jumanne 2 Februari 2016.

Katika michuano ya CECAFA Senior Challenge mwaka jana nchini Ethiopia, Tuyisenge, 24, alicheka na nyavu mara 3 kwa Amavubi licha ya ushindani mkubwa uliokuwepo. Tangu ajiunge na Rwanda Police msimu wa majira ya joto 2012 kutoka SC Kiyovu, msasi huyo wa magoli amekuwa katika 11 bora ya klabu hiyo na timu ya taifa. Hata hivyo kumlinganisha na Olunga, nyota aliyekwenda Sweden kwa majaribio baada ya kufungia Gor mabao 19 katika mechi 28 msimu uliopita, akicheza dakika 2, 472 na kuoneshwa kadi moja tu ya njano ni karibu na mzaha.

Micahel Olunga (kulia) katika mechi ya ligi kuu Kenya msimu wa 2015

Atarajie nini Tuyisenge?

Changamoto gani zinamsubiri Tuyisenge? Kwanza ni shinikizo kutoka kwa ”Green Army”, mashabiki wa Gor ambao daima watamlinganisha na kina Olunga na Kagere na kutaka azidishe makali yao. Asisahau msimu wa 20015 kombe la ligi kuu lilitua mikononi mwa Gor pasi kushindwa, klabu hiyo ikafika fainali ya klabu bingwa CECAFA, kashinda taji la KPL Top 8 na kuwahi fainali ya ngao ya GoTv, ufanisi wote huo ukizingirwa na uwezo wa kina Olunga. Atahitajika kufanya hivyo!

Mawio mema ni kuwa siku ya kuzinduliwa kwake udhamini wa Sport Pesa wa miaka 5 umetangazwa japo dau lake halijafichuliwa, hili litampa nguvu . Hata hivyo huenda akahitajika kufanya kazi bila mdhamini mustakabalini, kama watangulizi wake. Ikizingatiwa hatumiki katika mechi za klabu bingwa barani Afrika msimu huu, katika ligi kuu lazima ang’are apende asipende!

Tuyisenge karibu Kenya, ni ligi ya visa na visanga, bidii na uvumilivu muhimu sana ili kufaulu. Kila la kheri!

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here