Home Lifestyle “Wanaonitukana Instagram Fresh tu”- LULU

“Wanaonitukana Instagram Fresh tu”- LULU

Story zilivuma na bado vuguvugu linaendelea kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusu uhusiano wa staa wa kike katika filamu za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na mama Kanumba, Flora Mtegoa kuwa siyo mzuri kama zamani. Watoa habari wa mjini, wanadai kuwa mama Kanumba na Lulu kwa muda mrefu sasa hawapikiki chungu kimoja kama ilivyokuwa zamani. Lulu alikuwa mchumba wa mwigizaji wa filamu za Kibongo, marehemu Steven Kanumba ambaye alifariki dunia Jumamosi ya Aprili 07, 2012, nyumbani kwake, Sinza – Vatican jijini Dar es Salaam.
Mbali na mitandao ya kijamii kukuza kinachoitwa bifu kati ya mtu na mkwewe huyo, magazeti mbalimbali yalipata kuripoti kuhusiana na kuwepo kwa kutokuelewana baina yao.
Katika mahojiano na My Style ya Swaggaz ndani ya Mtanzania Jumamosi, Lulu alifunguka mengi kuhusiana na madai ya bifu hilo, akikiri kuwepo lakini akasema kuwa kwa sasa imebaki stori tu.
Akizungumzia hilo anasema: “Ni kweli kuna wakati kulitokea kutoelewana kidogo na naweza kusema ni jambo la kawaida. Jamani binadamu kutofautiana mitazamo wakati fulani si kitu cha kushangaza.
“Lakini hayo mambo yalishaisha kabisa. Mimi na mama Kanumba tupo vizuri sana kwa sasa. Sina ugomvi naye, tunaelewana na tunaishi vizuri kabisa. Mikwaruzano ya mwanzo iliisha na tunaendelea vyema.”
Lulu anawaangushia lawama watu wenye tabia za kukuza mambo mitandaoni ambao hawamtakii mema kwa kuzusha kuwa bado wana bifu.
“Tatizo kuna watu hawana kazi za kufanya, kazi yao kushinda mitandaoni na kutunga habari za uongo au kukuza mambo ambayo hayapo. Watu waache, mimi sina tatizo na mama Kanumba.
“Yule ni mtu mzima, nawezaje kuwa na bifu naye? Ninachoweza kusema ni kwamba kulikuwa na kupishana kauli kidogo, lakini hayo mambo yameshaisha, watu wasijaribu kuendelea kukuza,” anasema Lulu ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Africa Magic Viewer’s Choice Awards katika kipengele cha Filamu Bora ya Afrika Mashariki kupitia filamu yake ya Mapenzi ya Mungu ambayo mama Kanumba pia ameshiriki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here